Tuesday, July 17, 2012

BOLT NIMSHINDE, ANISHINDE SISI NI MARAFIKI TU - BLAKE

Sisi ni marafiki.... Yohan Blake (kushoto) na Usain Bolt.

YOHAN Blake amesisitiza kuwa urafiki wake na Mjamaica mwenzake, anayefanya naye mazoezi na ambaye pia ni mpinzani wake katika taji la dunia, Usain Bolt, utadumu kwa chochote kitakachotokea kwenye mashindano ya Olimpiki ya London 2012.

Blake alithibitisha kwamba atakuwa tishio kubwa zaidi kwa Bolt katika mbio za kuwania taji la mita 100 na mita 200 wakati alimpombwaga bingwa huyo wa Olimpiki katika mbio hizo zote mbili katika mashindano ya Jamaica.

"Kushinda, kushindwa au sare sisi ni marafiki, licha ya kwamba ni biashara na anataka kushinda nami pia nataka kushinda," alisema Blake.

Mbio za wanaume za mita 100 na mita 200 zitafanyika Agosti 5 na 9.

Kiwango cha Blake katika mbio za kwao Kingston mwishoni mwa Juni, kilimweka katika nafasi ya mrithi mtarajiwa na sio mpambe wa Bolt katika mbio zijazo London.

Blake ndiye bingwa wa dunia wa sasa katika mita 100 baada ya kushinda mbio za Daegu mwaka 2011 alipotumia sekunde 9.92, ingawa ushindi huo ulipatikana baada ya Bolt anayeshikilia rekodi ya dunia kuenguliwa kutokana na kukosea kuanza mbio.

Siku sita baadaye, Bolt alishinda mbio za mita 200 na kumhakikishia kuwa ni mtu anayepewa nafasi katika mbio zote mjini London.

Blake anaamini kwamba maamuzi yake ya kumtosa kocha wa shuleni Oktoba 2008 na kujiunga na Bolt chini ya kocha Glen Mills katika klabu ya riadha ya Racers Track Club ya mjini Kingston, Jamaica, kulimsaidia kumuinua.

"Kila wakati mazoezini nataka kushinda lakini daina amakuwepo pale. Hivyo nasema 'OK, nitashindaje katika siku ya siku?'" aliongeza Blake.

"Hii ndio maana wakati inapotokea niko mbele yake mashindanoni, huwa nasema  'OK, nilimshinda mazoezini'."
 

Bolt mwenyewe ana mchango mkubwa katika kumuinua Blake, ambaye amempachika jina la 'the Beast' na aliwahi kumtabiria mwaka 2009 kwamba atakuja kutawala.

"Aliniambia: 'Yohan, sikia, hufanyi mambo haya kwa ajili ya watu, unafanya hii kwa mashabiki, hufanyi hivi kwa ajili ya familia yako, unafanya kwa ajili yako mwenyewe.' Alikuwa akinipa ushawishi," aliongeza Blake.

Ushawishi si jambo ambalo Blake alilikosa.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 22 ni maarufu kwa tabia yake ya "kufia mazoezini" akijifua kwa nguvu na muda mrefu kuliko wapinzani wake wote, wakati moyo mweupe na kujiamini kwa Bolt kumekuwa ni sehemu ya mafanikio yake.

Bolt alitania kwamba anajitia mkosi kumtabiria Blake kuwa atashinda medali ya dhahabu kama yeye atashindwa kwenye Olimpiki.

"Tunafanya mazoezi kila siku, natambua anavyofanya mazoezi kwa bidii, hivyo ningependa Blake ashinde kama si mimi katika mita 100, lakini naomba msiulize tena swali hili, msinitie nuksi," alisema.

Matatizo ya kushindwa kuanza vyema kwa Bolt (25) yameendelea kuashiria presha aliyonayo nyota huyo ya kuendelea kuongoza inaonekana uwanjani na hata kwenye mikutano na wanahabari.

No comments:

Post a Comment