Monday, July 2, 2012

BOLT ABWAGWA TENA NA BLAKE MITA 200


Usain Bolt

KINGSTON, Jamaica
USAIN Bolt amebwagwa na Yohan Blake katika fainali ya mbio za mita 200 za kusaka bingwa wa Jamaica za kufuzu kwa michuano ya Olimpiki - ikiwa ni mara ya pili kwa mkimbiaji huyo anayeshikilia rekodi ya dunia kubwagwa na mpinzani wake huyo ndani ya saa 48.

Blake alimshinda Bolt katika mbio za mita 100 Ijumaa na akarudia jambo hilo katika mbio ndefu, akitumia sekunde 19.80, ambazo ni sekunde 0.03 mbele ya Bolt.

Bingwa wa dunia wa sasa wa mita 100 Blake alianza kuongoza wakati wa kukata kona, kisha akamuacha patna wake huyo ambaye anafanya naye mazoezi na kutwaa ubingwa wa taifa.
"Ninalazimika kuangalia nini nilikosea na kufanyia kazi," alisema Bolt.

Wakimbiaji hao wanatarajiwa kukutana tena katika mbio za Olimpiki mjini London.

Blake (22), alikuwa na kasi zaidi katika mbio za nusu fainali Jumamosi, akitumia sekunde 19.93, wakati Bolt alishinda mbio za kupasha moto misuli kwa kutumia sekunde 20.26.

Wao sasa ndio watu wenye kasi zaidi duniani walio hai katika mbio za umbali huo na vita yao inatarajiwa kuwa gumzo katika mbio za Olimpiki.

No comments:

Post a Comment