Monday, July 16, 2012

BERBATOV: FERGUSON ANANIUZA KWA BIL. 12/-


Dimitar Berbatov
LONDON, England
Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson yuko tayari kumuuza mshambuliaji aiye na nafasi katika kikosi chake, Dimitar Berbatov kwa dau la paundi za England milioni 5 (Sh. bilioni 12), mchezaji huyo raia wa Bulgaria amesema.

Berbatov, aliyeifungia Bulgaria mabao 48, amepoteza nafasi yake ya kuwemo katika kikosi cha kwanza cha Man U ingawa klabu yake ilichagua kuendelea kuwa naye kwa mwaka mmoja zaidi katika mkataba wake mwezi Machi. Alijiunga Man U akitokea Tottenham Hotspur mwaka 2008 kwa ada ya uhamisho ya paundi za England milioni 30.7 (Sh. bilioni 60).

"Nimesoma magazeti na kuona wakisema kwamba paundi za England milioni 10 ndio bei yangu. Nilienda na kuzungumza na Sir Alex, na kuniambia kwamba yuko tayari kuniuza kwa paundi milioni tano," Berbatov mwenye miaka 31 aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.

"Kwahiyo nani anasema kweli, nyie mnafikiri ni nani? Naipenda klabu hii lakini siwezi kuwa na msaada kwa yeyote yule kama sichezi. Na mimi ninataka kucheza.
"Lakini kwa sababu zisizofahamika, hilo halitatokea, au nafasi yangu itakuwa ndogo, kwahiyo itakuwa vizuri zaidi kwa pande zote kama tutaagana."

Berbatov alifunga mabao 14 katika msimu wake wa kwanza wa kuichezea Man U na akafunga mabao 12 katika msimu wake wa pili kabla ya kuwa kinara wa kupachika mabao katika Ligi Kuu ya England kwenye msimu uliofuata baada ya kupachika mabao 22.

Hata hivyo, msimu uliopita alijikuta akiachwa nje na Wayne Rooney, Danny Welbeck na Javier Hernandez katika kikosi cha kwanza baada ya Ferguson kukiri mwanzo wa mwaka huu kuwa kamwe hataweza kumhakikishia Mbulgaria huyo namba ya kudumu kwenye kikosi chake cha kwanza.

No comments:

Post a Comment