Monday, July 16, 2012

AMIR KHAN: NIMEDUNDWA LAKINI SIJIUZULU

Amir Khan wa Uingereza akitibiwa baada ya kupoteza pambano lake dhidi ya bingwa wa WBC, Danny Garcia wa Marekani katika pambano lao la ubingwa wa mataji ya WBC/WBA light-welterweight kwenye ukumbi wa Mandalay Bay Events Center mjini Las Vegas, Nevada Jumapili asubuhi. Picha: REUTERS

Amir Khan akijikongoja kunyanyuka kutoka 'sakafuni' baada ya kudondoshwa na Danny Garcia huku refa Kenny Bayless akimpelekea Garcia kwenye kona wakati wa pambano lao la ubingwa wa mataji ya WBC/WBA light-welterweight kwenye ukumbi wa Mandalay Bay Events Center mjini Las Vegas, Nevada Jumapili asubuhi. Picha: REUTERS

BONDIA wa Uingereza, Amir Khan amepuuza mitazamo kwamba anapaswa kustaafu ndondi baada ya kupoteza taji lake la WBA light-welterweight kufuatia kipigo cha raundi ya nne dhidi ya Danny Garcia.

Bingwa wa IBF super-middleweight, Carl Froch alikaririwa akisema kama angekuwa ni yeye angestaafu ndondi kama angepigwa kwa staili kama ya Khan.

Lakini bondia huyo wa Bolton (25), aliiambia BBC Sport: "Sizungumzii kuhusu kustaafu, mimi bado ni kijana mdogo, nina mengi kutoka kwangu.

"Bado nina njaa na nitarejea nikiwa vyema na mkali zaidi."

Kilikuwa ni kipigo cha tatu katika maisha ya Khan kufuatia kudundwa katika raundi ya kwanza dhidi ya Breidis Prescott mwaka 2008 na kwa pointi dhidi ya Lamont Peterson Desemba.

Froch alisema wikiendi: "Khan amepigwa na mtu ambaye si miongoni mwa mabondia wa kiwango cha juu. Inauma sana. Ningejiuzulu kama lingetokea kwangu."

Lakini Khan amejibu: "Carl daima hakosi cha kusema na ninamuacha kama alivyo. Kama anataka kustaafu, astaafu tu.

"Niko katika uzito ambao una ushindani zaidi, napigana na mabondia bora na mimi nina jina kubwa kuliko yeye. Hicho ndicho kinachomuuma.

"Watu watasema mambo baada ya pambano hili, lakini watu walisema mengi baada ya pambano langu dhidi ya Prescott na mliona nilivyorejea baada ya pale."

Kabla ya pambano la Jumapili asubuhi, Khan alizungumzia mipango ya kuongeza uzito hadi welterweight ili apambane na Mmarekani ambaye hajawahi kupigwa Floyd Mayweather.

Lakini sasa amekiri kwamba anatarajia kubaki katika uzito wa light-welterweight kwa angalau pambano moja zaidi.

"Inarudisha nyuma," alifafanua. "Niliingia katika uzito huu vyema na sasa naona ni vyema nibaki hapa kwa pambano moja zaidi - kama nitatwaa ubingwa kisha nitapanda uzito. Sina haraka.

"Watu wanaona kwamba 'Amir anapaswa kupanda uzito, kufanya hivi, kufanya vile'. Watu wanasahau umri wangu. Mimi bado ni kijana na nina mengi ya kufanyia kazi kabla ya kupanda ngazi ya juu.

"Tunafanyia kazi uwezekano wa kupata pambano la marudiano. Sijui kama watakubali, lakini kama tutapata pambano hilo England itakuwa poa sana."

Khan alisisitiza kwamba hana "cha kujutia" ukiacha ngumi ya kushoto iliyompele chini katika raundi ya tatu.

Kocha wake Freddie Roach anaona kwamba bondia wake anaweza kurejea kutoka katika fadhaa hiyo, lakini Khan alidokeza kwamba atachunguza mahusiano yao kama aendelee kufundishwa naye.

No comments:

Post a Comment