Thursday, July 12, 2012

ALIYEANDIKA 'MISTARI' YA BONGOFLEVA KWENYE KARATASI YA MAJIBU MTIHANI WA FORM IV AFUNGUKA

Watangazaji wa kipindi cha "Power Breakfast" cha Clouds FM, Gerald Hando (kulia), Paul James (katikati) na Barbara Hassan.

Na Mwandishi Wetu
KIJANA Julius Dawson (23), mkazi wa Tabata Segerea, ambaye mwaka jana alikuwa gumzo kufuatia kuandika "mistari ya Bongofleva" katika karatasi yake ya kujibia mtihani wa kidato cha nne, amefunguka kuhusu sababu ya kufanya jambo hilo lililoonekana kituko cha mwaka.


Dawson, ambaye asili yake ni Moshi Marangu, anayeishi peke yake Tabata baada ya baba yake kufariki huku mama yake akiwa anaishi Kisarawe, alisema lengo la kufanya vile ilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii ili kuokoa maisha ya vijana wengi kutokana na mfumo uliopo sasa ambao unamlazimisha kila kijana kuufuata bila ya kuwepo na mfumo mbadala.


Akizungumza kwa kujiamini wakati akihojiwa na mtangazaji Gerald Hando wa kipindi cha "Power Breakfast" cha Radio Clouds FM, Dawson, alisema mfumo mmoja wa maisha unawaharibia maisha vijana wengi ambao hawawezi kufiti katika mfumo huo, ambao pengine wangeweza kufanikiwa kama kungekuwa na mifumo mbadala.


"Waulize watu hawa wanaotamba katika muziki au umiss, utakuta wazazi wao walikuwa wanawakimbiza sana "huyu hataki shule", lakini akishafanikiwa utamsikia mzazi huyo huyo akisema "Mungu kamjaalia mwanangu kafanikiwa katika muziki". Sasa kama mzazi angemsapoti tangu mapema si angefanikiwa zaidi kuliko kumpotezea muda wake?" Alisema na kuhoji Dawson.
"Tatizo la nchi yetu ni kwamba kuna 'system' moja iliyowekwa, kwamba usipoifuata huna 'option' nyingine. Wakati naandika vile nilikuwa na lengo la kutuma ujumbe kwa watu wanaosimamia elimu hii kwamba kuna umuhimu wa kuwekwa kwa hizi 'system' tofauti za maisha kwa sababu mtu anaweza akawa si mzuri katika 'system' yao lakini akawa mzuri katika 'system' nyingine. Hivyo ziwepo ili wazazi waokoe pesa na muda wa kulazimisha kumpeleka mtu katika kitu ambacho mtu huko si mzuri.


"Ujumbe wangu ni kwamba wazazi na jamii itambue vipaji vya vijana wao. Inapotokea mtoto tangu mdogo ana kipaji cha kuimba ama kuigiza, ni vyema akasomea kitu ambacho kiko ndani yake.  
Mimi ni mmoja wa watu ambao wana maisha magumu wako mitaani kwa sababu tu tumeshindwa kwenda na 'system' yao. Unakuta vijana wana vipaji vingine ambavyo vingeweza kuwafanya wakaishi maisha bora kabisa.


"Nilipoandika jambo lile nilikuwa na maana yangu kubwa ya kufikisha ujumbe. Lakini ilivyopokewa ilikuwa tofauti. Watu walikuwa wakiangalia upande mmoja tu. Na ilikuwa inaniumiza sana. Kwa mfano nilikuwa ninaweza kuingia kwenye daladala, nikakuta watu wanaongelea jambo lile na wanaponda sana. Mimi nilikuwa najumuika nao kama mchangiaji mwingine. Nilikuwa nawaeleza kama haya ninayosasema hapa."


Wakati Hando alipomuuliza leo anajisikiaje kupata fursa ya kutoa ufafanuzi hewani, Dawson alisema: "Katika siku ninayojisikia furaha maishani, ni leo. Najiona kama mtu ambaye nimeutua mzigo uliokuwa ukimuelemea. Baada ya hapa hata nikiambiwa kufa, ni sawa tu kwa sababu nimeshautua mzigo."

Dawson pia alitumia fursa hiyo kuiomba radhi jamii kama aliikwaza ama kumkatisha tamaa yeyote kutokana na kitendo chake kile.


"Maoni yangu ni kwamba jamii iwasapoti watu kufanya kitu wanachokiweza. Mwisho kama kuna mtu ama mzazi nilimkwaza ama nilimkatisha tamaa, namuomba radhi. Mimi si 'bad boy', mimi ni kijana mwema kabisa."

Akielezea historia yake na kilichosababisha kuchelewa kumaliza kidato cha nne akiwa na umri mkubwa, Dawson alisema masomo yalikuwa yakimuwia ugumu na hivyo kumfanya arudie rudie shule.

"Nilianza shule msingi Umoja Mabibo mwaka 1996, lakini maisha yalikuwa magumu hapa mjini hivyo tukiwa na wazazi tukahamia Kisarawe.

"Mwaka 2002 nikachaguliwa kujiunga na Sekondari Manerumango. Wakati nikiwa kidato cha pili nikafeli mara mbili. Mara ya kwanza nilirudia, lakini mara ya pili nikaacha shule. 


"Baadaye mama yangu mdogo akanichukua nikaja huku Dar kusoma. Nikarudia tena shule baada ya kukaa nje ya masomo kwa miaka minne.

"Shule nilikuwa naipenda. Lakini aina ya elimu niliyokuwa naipata naona ilikuwa ngumu kwangu. Nilikuwa nachukua masomo ya biashara. Nadhani ugumu niliuona kutokana na jinsi nilivyoumbwa tu. Nilikuwa nasukumwa pia na mama yangu mkubwa. Maksi zangu zilikuwa za chini sana. Mwisho ndio nikamaliza kidato cha nne mwaka jana."


Alisema baada ya kufikisha ujumbe, sasa anajisikia huru licha ya kwamba hana kazi ya kufanya ya kumuingizia kipato.

"Nimerekodi wimbo mmoja unaitwa "Mr President" unaongelea upande wa rais anayetolea majibu maswali ya wananchi na huku pia akielezea ugumu wa kazi yake. 

"Nimeurekodi katika studio ya prodyuza mzungu Fundi Samweli wa Kibaha na kisanii natumia jina la "Elinaja". 

Katika sehemu ya mistari yake, Dawson anaimba: "Mnasema Mr President kila mahala kajaza rafiki zake, ni nani kati yetu anashirikiana na maadui zake." 

Na kiitikio kinasema: "Wanagomba wanasumbua kila tatizo nasemwa mimi, mara "Mjomba" mara "Mshua" oooh Mr President." Jina la Mjomba lilitumika katika nyimbo za Mrisho Mpoto wakati neno "Mshua" lilitajwa katika wimbo 'Rizi-One' wa rapa Izzo Bizness.

Dawson a.k.a Elinaja alisema amerekodi wimbo huo kwa fedha za kuunga-unga kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki.


"Nina nyimbo za kutosha albam nzima. Tatizo ni pesa. Naomba jamii inisaidie kufanikisha ndoto yangu," alisema kijana huyo ambaye aliwafanya waandishi wa habari waangue vicheko mwaka jana wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Joyce Ndalichako, alipoisoma "mistari" yake ya Bongofleva, wakati akitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.

Baada ya mahojiano ya Dawson na Hando, watu mbalimbali walituma ujumbe radioni Clouds FM kuonyesha sapoti yao kwa kijana huyo akiwamo Salum Mwalimu wa Vodacom na Jackson Mbado wa Airtel, huku Salum Mwalimu akimuita kuwa ni shujaa wake.

No comments:

Post a Comment