Friday, July 13, 2012

AKAMATWA TUHUMA ZA KUMTEKA DKT. ULIMBOKA

Dkt Ulimboka

Na Mwandishi Wetu
MTUHUMIWA wa kwanza wa tukio tata la kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, amekamatwa.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema leo kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa baada ya kwenda kanisani kwa nia ya kuungama kutokana na kuhusika kwake na tukio hilo.Alisema mtu huyo aitwaye Joshua Gitu Mhindi mwenye umri wa miaka 31, ana kitambulisho cha utaifa Na.29166938 kilichotolewa Nyeri na hati ya kusafiria ya dharura Na.0123431 iliyotolewa Namanga Kenya.

Alisema katika maelezo yake, mtuhumiwa huyo alisema alitumwa kufanya jambo hilo pamoja na wenzake 12 na bosi ambaye hafahamu kama ni kigogo wa serikalini.

Kamanda Kova alisema mtu huyo alieleza kuwa yeye ametokea katika kundi la Kenya linaloitwa Gun Star linalojihusisha na utekaji, utesaji na ubakaji linaloongozwa na mtu anayeitwa "Silencer".

Kova alisema wanaendelea kumshikilia mtu huyo na kufanyia kazi maelezo yake wakati wakiendelea kuwasaka watuhumiwa wengine.

Aidha, Kamanda Kova amepiga marufuku maandamano yoyote yaliyopangwa kufanywa kesho akisema hayajaruhusiwa.

"Kama ni ya kikundi cha Kiislamu ama ya madaktari, maandamano yoyote yaliyopangwa kufanyika si halali," alisema Kamanda Kova.

Suala la kutekwa na kuteswa kwa Dkt. Ulimboka limekuwa gumzo kubwa nchi nzima huku bungeni nako kukiwaka moto kwa wabunge hasa wa upinzani wakitaka iundwe tume huru ya kuchunguza tukio hilo la utata.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alisema kuwa serikali haioni sababu ya Bunge kuunda tume huru ya kuchunguza ukweli kuhusu unyama aliofanyiwa Dkt. Ulimboka kwa vile tayari suala hilo linashughulikiwa na vyombo husika.

Mkuchika alitoa maelezo hayo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati wa kuhitimisha mjadala kuhusu makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Mapema, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi a.k.a Mr II Sugu, alitaka iundwe tume huru ya kuchunguza ukweli kuhusu utekaji na unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka ambaye alikimbiziwa Afrika Kusini na baadaye kuripotiwa kupelekwa Ujerumani kuendelea na matibabu kwa vile Serikali haiaminiki kuhusiana na jambo hilo. Alilifananisha pia tukio hilo na unyama unaofanywa nchini Sudan na kikundi kinachotesa na kufanya mauaji dhidi ya wananchi cha ‘Janjaweed’.

Akiendelea kufafanua, Mkuchika alieleza kwamba Serikali inarudia tena kulaani tukio la kutekwa na kushambuliwa kwa Dk. Ulimboka, lakini akakana madai kuwa Serikali haiaminiki kama alivyosema Sugu kwavile matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita (mwaka 2010) yalidhihirisha ni kwa kiasi gani serikali (ya CCM) inavyoaminika kwa wananchi.

Hivi karibuni, Dk. Ulimboka aliyekuwa miongoni mwa vinara wa mgomo wa madaktari alizua gumzo kubwa baada ya kukumbwa na tukio la kutekwa, kushambuliwa kinyama na kisha kutupwa kwenye msitu wa Mabwe Pande jijini Dar es Salaam. Hadi sasa haijajulikana wazi kuwa ni watu gani waliohusika na tukio hilo.

Wakati wa hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alisema haya hapa chini kuhusu Suala la Dkt. Steven Ulimboka:

Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012.
Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo.
Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. 
Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka.
 Mimi nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo.
 Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na Madkatari. 
Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.
 Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.

Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana. 
Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana. 
Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa. 
Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo. 
Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.
 Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru?  Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na Serikali.

Ndugu Wananchi;
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa.  Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini.  Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. 
Muwe na moyo wa huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment