Tuesday, June 26, 2012

CASILLAS: RONALDO BADO HAJAONYESHA KIWANGO CHAKE EURO 2012

Casillas
Ronaldo

GNIEWINO, Poland
NAHODHA wa timu ya taifa ya Hispania, kipa Iker Casillas amesema kuwa mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Ureno bado hajaonyesha kiwango chake alichoonyesha msimu uliomalizika katika klabu anayocheza naye pamoja ya Real Madrid.

Casillas ambaye anafukuzia rekodi ya ushindi wa 100 akiwa na jezi ya Hispania wakati watakapocheza dhidi ya Ureno katika nusu fainali ya kwanza ya Euro 2012 kesho, alisema kwamba kwa mtazamo wake, Ronaldo aliyeifikisha Ureno nusu fainali kutokana na mabao matatu yaliyomuweka kileleni mwa orodha ya wafungaji wa michuano hiyo hadi sasa si yule aliyetisha Real Madrid na kuwapa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne.

"Alikuwa na msimu mzuri Real Madrid kutokana na namna alivyocheza, mabao aliyofunga na rekodi alizoweka," kipa huyo mwenye miaka 31, anayefahamika zaidi Hispania kama "Saint Iker" kutokana na uwezo wake wa kuokoa kiajabu michomo ya hatari kutoka karibu na lango, alikaririwa akisema juzi na katika gazeti la michezo la kila siku la Marca.

"Sidhani kama hivi sasa anacheza katika kiwango chake cha juu," aliongeza.

Ronaldo amekuwa mhimili wa Ureno kutokana na kasi yake inayosumbua mabeki wa upinzani na pia mabao yaliyoifikisha Ureno katika hatua ya nusu fainali ya Euro 2012.

No comments:

Post a Comment