Tuesday, June 26, 2012

ARSENAL YAMSAINISHA OLIVIER GIROUD

 

Olivier Giroud
LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Olivier Giroud amejiunga na Arsenal kwa mkataba wa muda mrefu, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England ilisema leo.

Mchezaji huyo mwenye miaka 25 alikamilisha kuchukuliwa vipimo vya afya kwenye klabu hiyo juzi na kukubaliana na yaliyomo katika mkataba wake utakaoanza rasmi Julai Mosi, Arsenal iliongeza katika taarifa waliyotoa kupitia tovuti yao (www.arsenal.com)

"Kukamilika kwa uhamisho wake sasa ni suala tu la utaratibu wa mchakato wenyewe," iliongeza klabu hiyo ya jiji la London, iliyomaliza kwenye nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya England msimu uliopita na kutwaa nafasi ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Giroud ametua Arsenal akitokea kwa mabingwa wa Ufaransa, Montpellier baada ya kuichezea timu ya taifa lake katika fainali za Euro 2012 nchini Poland na Ukraine.

Mabao yake 21 katika mechi 36 yalimfanya amalize kileleni mwa orodha ya wafungaji wa Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa msimu uliopita akiwa pamoja na Nene wa klabu ya Paris St Germain.

"Tumefurahi kumsajili Olivier Giroud," alisema kocha wa Arsenal, Mfaransa Arsene Wenger.

"Ana umbile zuri la soka, ni mkali wa mipira ya juu na pia hucheza kwa kujituma.

"Tunayo furaha kubwa kuhusiana na Olivier kujiunga nasi na ataongeza idadi ya washambuliaji tunaoweza kuwatumia msimu ujao."

Giroud alisema kwamba ndoto yake ilikuwa ni kucheza katika Ligi Kuu ya England na alivutiwa na Arsenal kutokana na falsafa yao ya soka na pia umaarufu wa Wenger.

No comments:

Post a Comment