Saturday, June 30, 2012

NIMEBAKWA NA WANAUME WATANO WALIOVAA KIJESHI DRC, WATANZANIA WAMENITIBU

Charlie Mokuta akiimba shairi akiomba suluhu ya kudumu dhidi ya ubakaji na utesaji mjini Kampala hivi karibuni. Picha: Abubaker Lubowa 

Na Sarah Tumwebaze
UTANGULIZI:
Charlie Mokuta alibakwa na wanaume watano, wote wakiwa wamevalia kijeshi, ambao walimtuhumu kuficha taarifa kuhusu rais wa wakati huo wa Congo, Mobutu Mobutu Sese Seko, kufuatia kungolewa kwake. Mwanamama huyo alikimbilia Uganda kuanza maisha mapya.

CHARLIE Mokuta alighani shairi kwa lugha ya Kifaransa, sikuweza kuelewa alichokuwa akikisema. Hata hivyo, mwonekano wa sura yake ulionyesha kwamba alikuwa katika hisia za machungu. Baadaye nikatambua kilichomo kwenye shairi lile, Mokuta alikuwa akiomba suluhisho la kudumu dhidi ya utesaji na uhalifu wa kimapenzi.

Aliliandika kutokana na uzoefu wa yaliyomkuta mwenyewe na alichoona wakati wa vita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo zamani ilijulikana kama Zaire.

"Watu walikuwa wakifa na kukumbana na uhalifu usio na sababu, wote wanaume kwa wanawake walikuwa wakililia walichopoteza. Hivyo nikatunga shairi hili kuzungumzia jambo hilo," Mokuta alifafanua huku akijaribu kuweka tabasamu lililogoma kutokana na kumbukumbu mbaya.

Mjane huyo mwenye umri wa miaka 45 alikimbilia Uganda Novemba mwaka jana baada ya kubaini kwamba ndugu wa mmoja rafiki zake alikuwa akimsaka akitaka kumuua akimtuhumu alimuua shogaye huyo.

"Alikuwa akinituhumu kwa kifo cha dada yake ingawa sikuhusika nacho."

Mokuta anasema kwa mara ya kwanza kuteswa ilikuwa ni kipindi cha mabadiliko ya utawala kutoka kwa rais Mobutu Sese Seko.

"Nilikuwa mfakanyazi wa Ikulu ya Congo wakati Mobutu aling'olewa madarakani mwaka 1997. Wakati Laurent Kabila alipoingia madarakani, nilitupwa gerezani. Wakati nikiwa kule, nilipigwa na kuteswa sana."

"Wanajeshi walidhani nilikuwa na taarifa kuhusu serikali iliyopita. Lakini baada ya kubaini kwamba nilikuwa sina hatia, waliniachia."

Alipotoka gerezani, alianza kufanya kazi katika wizara ya madini. "Nilikuwa nikiishi maisha mazuri. Nilikuwa na magari na nyumba nzuri sana. Ingawa mume wangu aliuawa vitani, nilikuwa na pesa ya kuwalea vyema watoto wetu watano."

Hata hivyo, katika siku ya tukio baya zaidi maishani mwake Machi 2011, wizara hiyo ilivamiwa na watu waliovalia sare za jeshi.

"Mwenzangu alipowaona, alibeba pesa tulizokusanya siku hiyo (dola 42,000 sawa na Sh. milioni 65) na akaenda kuzificha. Lakini nadhani wanaume wale walimuona."

SHAMBULIO
Alisema walipoingia ofisini, wanaume hao walitaka pesa, wakajibiwa kuwa pesa zimepelekwa benki.

"Walifyatua risasi pembeni yake (shoga yangu) na kumwambia akalete pesa kutoka alikoenda kuzificha. Mara ya kwanza alikataa lakini walimkata mkononi, akanyanyuka kwenda kuzileta pesa," Mokuta alifafanua. Aliongeza kuwa baada ya kupata pesa, walimninia risasi kadhaa wakamuua.

"Walikuwa wanaume 15 jumla. Hivyo wakati wengine wakipakia fedha, wengine watano wakanijia mahala nilipokuwa. Mmoja wao akataka kunibaka. Lakini nikapambana naye. wakati nikiendelea, wale wengine wanne wakaingilia wakawa wakinikata ngozi yangu kwa mapanga maeneo ya kiwiko."

Kutokana na maumivu aliyokuwa akipata kutokana na kukatwa pamoja na makofi na mateke aliyokuwa akiendelea kupata kutoka kwa wanaume hao ambao pia walimtwanga kwa vitako vya bunduki, Mokuta hakuweza kupambana tena.

"Nikabakwa na wanajeshi wote watano; ambao huku walikuwa wakinitemea mate usoni, wakinitania ninavyoumia na kunitaka nijiokoe. Sikuwa na msaada na nilichoweza kufanya ni kulia tu."

"Baada ya kunibaka, mmoja wao akachukua panga lake na kunikata ndani ya sehemu zangu za siri. Wote wakacheka na kuondoka wakiniacha navuja damu kupindukia. Wakati nikiugulia maumivu makubwa, nilikuwa nikiwafikiria watoto wangu tu, sikupenda kuwaacha peke yao duniani".

MAUMIVU
Kutokana na kuvuja damu sana na maumivu aliyokuwa akiyasikia kutokana na kipigo, Mokuta alipoteza fahamu. Alizinduka na kujikuta akiwa katika hospitali ya Kavu. Walimfanyia upasuaji na kumpa tiba lakini haikumsaidia kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.

Hata hivyo, wakati akiwa hospitali, kikundi cha Area Domestic Violence Committee (ADVC) kilimchukua na kumpeleka Tanzania kwa ajili ya matibabu zaidi. "Nilitibiwa Tanzania na nikapona kabisa. Hivyo nikarejea Congo."

Baada ya kurejea Congo, alikutana na taarifa mbaya.

"Niliambiwa kwamba kaka wa mmoja wa wafanyakazi wenzangu yule aliyeuawa na wanaume wale waliotuvamia ofisini kwetu alikuwa akinisaka. Alikuwa akisema kwamba nilipanga mauaji ya dada yake hivyo nami napaswa kufa. Niliogopa sana kwa sababu alikuwa ni mfanyakazi sekta ya ulinzi Congo. Hivyo nikaamua kujificha."
Hata hivyo, katika nchi iliyotawaliwa na vita hakuwa na mahala pa kwenda kujificha, Mokuta hakuwa na chaguo zaidi ya kukimbilia Uganda.

Wakati watu wengine wanakimbia mashambulio ya kihalifu nyumbani, mimi nililazimika kumkimbia mtu mmoja ambaye alikuwa akiniwinda kwa tuhuma kwamba nilimuua dada yake," alisema.

Nchini Uganda, alilazimika kupambana na vikwazo kadhaa. "Tulipofika kwenye mpaka wa Kisoro, nilikuwa na watoto wangu wote watano. Watu waliokuwa wakituorodhesha walikuwa wakitaka tuwape pesa, dhahabu ama tulale nao kabla hawajatusajili.

Hata hivyo tulifanikiwa kuwashawishi kwamba hatuna pesa wala dhahabu na kwamba hatuwezi kulala nao. Baadaye wakatusajili."

Mukota alisema alikaa katika kambi ya wakimbizi kwa muda mfupi kabla ya kuondoka. "Sikuyaweza maisha ya kambini. Unachofanya wewe ni kukaa tu na kusubiri chakula ambacho wakati mwingine hakitoshi. Hivyo nikaamua kuondoka na familia yangu kuja Kampala.”

MADAI YA RUSHWA
Hata hivyo, Waziri wa Kukabiliana na Majanga na Kusaidia Wakimbizi, Stephen Mallinga alisema madai ya Mukota kuhusu usajili wa wakimbizi ni ya uongo.

"Huo ni uongo, sijawahi kusikia matukio kama hayo katika kambi yoyote nchini."

Aliongeza kuwa Uganda ni moja ya nchi zenye sera bora ya wakimbizi. "Si kweli kwamba wakimbizi wanapata shida, hakika wanaishi katika mazingira mazuri."

Lakini Mokuta, ambaye ni mmoja wa wakimbizi zaidi ya 43,000 waliopo Uganda, anasema maisha si marahisi nchini nchini Uganda.

"Kuna vitu nilikuwa nikivichukulia poa kama mkate ama chakula cha ziada mezani, lakini jambo hilo halipo tena. Siwezi kupata kazi kwa sababu ya kikwazo cha lugha. Sasa ninalazimika kutegemea pesa kidogo zinazoletwa nyumbani na wanangu ambao wanafanya kazi za mikono."


CHANZO: Gazeti la Monitor Uganda

http://www.monitor.co.ug/News/National/Congolese+narrates+gang+rape+ordeal/-/688334/1439638/-/item/1/-/141bd4a/-/index.html

No comments:

Post a Comment