Sunday, June 24, 2012

NI MIAKA MITATU YA KIFO CHA MICHAEL JACKSON

*Kimwana wa 'Thriller' asema: Ninamuona Michael kila nikiamka

Ola Ray (kushoto) akiwa na Michael Jackson katika video ya mwaka 1983 ya 'Thriller'.


NEW YORK, Marekani
JUMATATU, itakuwa ni miaka mitatu tangu Mfalme wa Pop, Michael Jackson, alipofariki akiwa na umri wa miaka 50.

Ola Ray, kimwana wa video yake ya "Thriller" ya mwaka 1983, bado hawezi kusahau uzoefu alioupata kwa kufanyakazi na gwiji huyo.

Ray -- ambaye sasa ana umri wa miaka 51 na anaishi Sacramento, California, pamoja na bintiye mdogo -- alipata fursa ya kufanya kazi na Michael baada ya muigizaji Jennifer Beals kukataa. Na alikuwa nusura aikose nafasi hiyo baada ya muongozaji wa video hiyo ya Thriller, John Landis, kubaini kwamba alipiga picha za kujianika za jarida la Playboy mwaka 1980. Lakini Michael hakuona ubaya wa mambo yake ya zamani. "Alionekana kuvutiwa na ukweli kwamba nilikuwa kimwana wa Playboy," Ray aliliambia gazeti la Sunday Mirror.

Video hiyo ya kutisha ya dakika 13 -- ambayo Kitabu cha Rekodi za Dunia cha Guinness kiliita video ya muziki yenye mafanikio kuliko yoyote iliyopata kutokea, ambayo iliuza nakala milioni 9 -- iliwaonyesha wawili hao kama wapenzi. Ilibadilika kuwa hofu wakati muimbaji huyo alipobadilika kuwa dudu la kutisha.

Tangu siku ya kwanza, Ray alisema yeye na Jackson walikuwa wanaendana sana.

"Tulipokuwa tunadansi pamoja, tulipokuwa tukiongozana na alipokuwa akinichezea… Pale ndipo nilipojisikia 'Oh Mungu wangu, kama Ola, nilishindwa kuamini kama mimi ndiye msichana niliyechaguliwa,'" aliiambia ABC News katika mahojiano mwaka 2010.

Jackson pia alikuwa na utani mwingi nje ya kamera.

"Alinimbia mara kwa mara, 'nasubiri kwa hamu ufike ule wasaa wa kucheza kama dubu  ili nikukimbize,'" Ola alimweleza mwandishi Mark Bego kwa ajili ya kitabu chake cha On The Road With Michael.

Ingawa wawili hao walicheza kimahaba na kutumia muda wakiwa faragha wakati wa kuandaa video hiyo, Ola alisema hawakuwahi kuhusiana kimapenzi kwa sababu Jackson alikuwa akimpenda mwanamke mwingine.

"Tulikuwa na mahusiano ya kikazi, hapakuwa na zaidi ya hicho," aliiambia ABC News. "Alikuwa akimzimia Brooke Shields."

Ola na Jackson walibaki kuwa marafiki baada ya kutengeneza video hiyo. Jackson pia alisafiri kwenda Ujerumani kupokea tuzo ya "Thriller" — ambayo baadaye alimpa Ola akae nayo.

"Alitaka kumtuma mtu mwingine aje kuichukua (kutoka kwangu), lakini nilimwambia, 'Hapana. Kama hutakuja kuichukua wewe mwenyewe, basi hutoipata,'" alisema Ola, ambaye alikuja baadaye kupata nafasi ndogo za kucheza filamu katika filamu za "Beverly Hills Cop II," "Gimme A Break!" na "Cheers". "Hakuja kuichukua, hivyo alinipigia na kuniambia. Naweza kubaki nayo tu."

Wawili hao pia waliwahi kuwa na utata baina yao: Mwaka 2009, mwezi mmoja kabla Michael hajafariki, Ola alimshitaki akidai hakulipwa haki zake kutokana na video hiyo (wawili hao walimaliza tofauti hizo nje ya mahakama Mei 2012).

"Michael alikuwa akitoa Thriller katika matoleo tofauti mara kwa mara ili niweze kuendelea kupata gawio langu," alisema katika taarifa yake baada ya kifo cha Michael. "Alifanya kila awezalo kunisaidia wakati akiwa hai. Lakini ajabu, watu wake wanaosimamia mali zake hawajafanya kulingana na matakwa yake tangu alipofariki."

Hata hivyo, Jackson amemuachia alama kubwa maishani mwake.

"Nina picha kubwa la ukutani la Michael, lake mwenyewe na nina albamu ya picha zake za sherehe ya kutimiza miaka 25," aliiambia ABC News. "Pia nina picha inayotuonyesha sisi wawili tukitembea katika video ile  … namuona Michael kila ninapoamka asubuhi."

--------------

No comments:

Post a Comment