Friday, June 22, 2012

GULLIT, MKEWE WAZIDI KUSHUTUMIANA

*Gullit asema: Nilijificha nyuma ya pipa kumfumania

Ruud Gullit na Estelle wakati wa ndoa yao mwaka 2000.

GWIJI wa soka Ruud Gullit amesimulia namna alivyomrekodi mkewe akimwita "mpuuzi" — na kisha alivyojificha nyuma ya pipa la taka kwenye uwanja wa ndege ili kumfumania akifanya udanganyifu wa kimapenzi.

Nyota huyo wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Uholanzi alishawishika kwamba Mwanamitindo wa Kidachi, Estelle, alikuwa na mahusiano ya nje ya ndoa na bingwa wa dunia wa kickboxing wa Morocco.

Gullit, 49, alinyata jikoni na kumsikia mkewe huyo ambaye ni wa tatu maishani mwake na mama mkwewe wakimsengenya na kumwita majina mabaya.

Baadaye, wakati Estelle, 33, alipokuwa akirejea kutoka mapumzikoni na rafikiye huko Ibiza, mchambuzi huyo wa soka katika kituo cha televisheni cha Sky Sports alijificha nyuma ya pipa la taka wakati mkewe huyo alipokuwa akishuka kutoka kwenye ndege akitokea Marrakech, Morocco.

Gullit — ambaye amekiri kwamba hata yeye "hakuwa mtakatifu" linapokuja uaminifu wa ndoa — aliliambia gazeti la Uholanzi kwamba Estelle alikanusha kila jambo mpaka alipomuwekea mkanda aliomrekodi. Aliongeza: "Nilikuwa nikichekwa nyumbani kwangu mwenyewe. Niliona jambo hilo ni baya kuliko udanganyifu wa nje ya ndoa."

  'Handsome Boy' aliyemchanganya mke wa Gullit, Badr Hari, ambaye anatajwa katika orodha ya wanaume wenye mvuto zaidi wa nchi za Mashariki ya Kati.
Mama wa watoto wawili Estelle, ambaye ni mpwa wa gwiji wa soka wa Uholanzi, Johan Cruyff, hivi karibuni aliondoka nyumbani kwa Gullit na kuhamia kwa nyota wa kickboxing, Badr Hari, 28, huku akimtuhumu Gullit kuwa na mahusiano nje ya ndoa.

Estelle, 33, alidai kwamba Gullit alikuwa na wanawake wengi nje ya ndoa na ndicho kilichomfanya aondoke kwenda kwa "kickboxer" huyo, ambaye ni mdogo kwa miaka 21 kwa Gullit.

Mwanamama huyo aliliambia gazeti la De Telegraaf kwamba usaliti wa ndoa yao uliokuwa ukifanywa na mumewe ndio chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yao iliyodumu kwa miaka 12.

Estelle alisema: "Hakika Ruud alikuwa na mahusiano nje ya ndoa. Daima alikuwa akifanya hivyo katika kipindi cha ndoa yetu. Na hakika nilifahamu kuhusu wanawake wake.

"Na hakika aliwakana kila siku. Uaminifu wangu kwake ulizidi kupungua kwa kadri miaka ilivyokuwa ikienda. Mwisho nikawa simuamini hata punje.

"Hicho ndicho kipindi nilichoanza kujiuliza mwenyewe, ndoa hii imeegemea wapi?”

"Nilikuwa nikiweka tabasamu 'la plastiki' kwa rafiki zake kwa muda mrefu."

Estelle amedai kuwa Ruud, 49, alishangazwa wakati alipomweleza kwamba anataka talaka.

Mwanamama huyo alisema: "Ruud amekasirika na kuchanganyikiwa. Anashinda kuamini kinachotokea. Alikuwa na hasira zaidi nilipomueleza kwamba naondoka."

Ruud aliviambia vyombo vya habari vya Uholanzi wiki hii kwamba anatalikiana na mkewe "kutokana na mambo yanayoendelea kutokea katika ndoa yake".

Wawili hao walifunga ndoa mwaka 2000 baada ya miaka minne ya kuwa pamoja kama wapenzi. Mahusiano yao yalianza wakati Estelle akiwa na umri wa miaka 17 tu.

No comments:

Post a Comment